Leo hii niko Morogoro mji kasoro bahari , naam kwa mbali nikiwa katika milima ya uluguru nikipasha viungo kwa mbali nasikia watoto, wazee, vijana , waume kwa wake wakiliimba jina la @Rambo. Rambio Rambo hakika jina la Rambo halitamkwi kama jina la mtu wa kawaida. Linatajwa kama simulizi, kama historia, kama alama ya ujasiri uliovuka mipaka ya hofu na jinsia. Ni jina linalotangulia heshima kabla hata mhusika hajafika. Si kwa sababu ya cheo, bali kwa sababu ya matendo. Si kwa kelele, bali kwa ujasiri uliothibitishwa kwa vitendo.
Huyu alikuwa Sajenti wa Jeshi la Polisi Tanzania, askari wa kike aliyevaa sare si kwa mapambo, bali kwa dhamira. Aliivaa kwa kiapo cha kulinda wanyonge, kuokoa wasio na hatia, na kukabiliana uso kwa uso na giza ili wengine waishi kwenye mwanga. Ndiyo maana watu waliposema, “Hawa ndio Polisi wetu, Mungu awalinde,” walimaanisha yeye.
Rambo hakuwa askari wa kusubiri maagizo. Alikuwa askari wa kujituma. Askari wa mstari wa mbele. Pale hatari ilipo, hapo ndipo alipokanyaga bila kuangalia nyuma. Jinsia haikumzuia, hofu haikumzuia, na mazingira hayakumlegeza. Alikuwa mpiga masumbwi hodari, mtaalamu wa judo na karate, fundi stadi wa magari na pikipiki, na dereva aliyekuwa anaaminiwa kwenye operesheni nzito za kiusalama. Alijua bunduki, aliujua kuulinda mwili wake, na zaidi ya yote, alijua thamani ya uhai wa mtu mwingine.
Akiwa katika kikosi cha Voda Faster, Rambo alikutana ana kwa ana na uporaji, ujambazi, na mapambano yaliyomuweka katikati ya hatari mara nyingi. Aliingia misituni akiwa na AK-47 kifuani, risasi begani, na kisu mkononi si kwa ajili ya sifa, bali kwa lengo moja kuu: kuhakikisha raia wanarudi salama majumbani mwao. Wengi waliishi, wengi waliokolewa, kwa sababu mwanamke huyu hakusita pale wengine waliposita. “Hao ndio Polisi wetu,” jamii ilisema kwa sauti ya imani.
Tukio moja lilibaki kama alama isiyofutika katika historia ya ujasiri wake. Pale pori la Melela–Kibaoni, gari lake liliharibika katikati ya mapambano dhidi ya majambazi. Hali ilikuwa mbaya. Hatari ilikuwa wazi. Lakini Rambo hakukata tamaa. Alitumia akili kabla ya nguvu. Alibadilisha mbinu, akabadilisha mavazi, akavaa dela na kujifanya mama ntilie. Majambazi waliporudi barabarani, aliomba lift ndani ya gari lao, katikati ya pori la Iyovi. Ilikuwa ni mbinu ya kipekee, hatari, lakini ilifanikiwa. Jamii ilishangilia, jeshi la polisi lilipongezwa , na historia ikaandikwa.
Lakini ujasiri wake haukuwa wa silaha pekee. Alikuwa muokoaji wa kweli. Aliwaokoa vijana waliolazimishwa kufanya uhalifu porini. Aliwatoa madereva bodaboda kwenye mitego ya dawa za kulevya. Aliwasimamia wanawake waliokumbwa na ukatili wa kijinsia, udanganyifu, na unyonyaji. Kwa wengine alikuwa askari; kwa wengi alikuwa dada, mama, rafiki, na sauti ya matumaini.
Rambo alipokuwa Trafic, aliwahi maeneo ya ajali kabla ya wengi. Alifunga damu, aliwahisha majeruhi hospitalini bodaboda, magari madogo, hadi malori makubwa. Katika ajali kubwa ya lori la mafuta lililolipuka Msamvu mwaka 2019, alihusika kuokoa majeruhi wengi. Wapo leo wanaotembea, wanaopumua, wanaoishi, kwa sababu Rambo alifika kwa wakati.
Ndani ya jamii, hasa kwa wana Morogoro, alikuwa kipenzi cha watu. Vijiwe vya bodaboda vilimjua kama rafiki na mshauri. Alihimiza helmet, kuonya mwendo kasi, na kusisitiza thamani ya maisha kuliko haraka. Alikuwa mcheshi na mchangamfu, lakini ucheshi wake haukumzuia kuwa askari makini na mwenye nidhamu ya kazi.
Kwa sababu ya ujasiri wake, ustadi wake wa mapambano, na uwezo wake wa kuingia hatarini ili wengine wawe salama, wananchi walimpa jina la kishujaa: @RAMBO. Jina hilo halikutoka kwenye filamu, bali kwenye uhalisia wa maisha aliyoyaishi.
Leo, simulizi hii inauma zaidi. Rambo hayupo tena. Ameaga dunia, na kuacha pengo kubwa katika mioyo ya wengi. Wanamorogoro wanamlia, bodaboda wanakumbuka, wanawake wanaomboleza, na sauti za huzuni zinasikika: “@RAMBO wetu katutoka.”
Lakini kifo chake hakijafuta alama zake. Ameacha mfano wa mwanamke jasiri, askari wa kweli, na binadamu aliyethamini maisha ya wengine kuliko yake. Jamii inamuombea apumzike kwa amani, ikitambua kuwa aliokoa wengi na kutenda mema mengi.
Mwandishi: Mr Elimu Jamii
No comments