Kuna wakati mwanamke hufikia hatua ya kufanya uamuzi mzito wa kuondoka kwenye uhusiano, si kwa sababu mapenzi yamekufa, bali kwa sababu matumaini yamechoka. Mara nyingi mwanamke huanza safari ya mapenzi akiwa na moyo safi, tayari kupenda, kuvumilia na kuamini. Hata hivyo, kadiri muda unavyopita na ahadi zinavyoendelea kutolewa bila kutekelezwa, mapenzi huanza kupoteza nguvu yake ya kumfanya abaki. Mwanamke anaweza kumpenda mwanaume kwa dhati, lakini bado akagundua kuwa mapenzi pekee hayawezi kujenga maisha yenye mwelekeo.
Kimsingi, mwanamke hufikiria zaidi kesho kuliko leo. Anaweza kuvumilia hali ngumu ya sasa, lakini hawezi kuvumilia kutokuwepo kwa mpango wa baadaye. Anapomuona mwanaume akibaki palepale, bila mipango, bila juhudi za kweli, na bila dhamira ya uwajibikaji, huanza kuona hatari ya kupoteza muda wake. Hapa ndipo moyo wake hulazimika kuchagua kati ya kuendelea kuishi kwenye ahadi au kuchagua uhalisia unaompa uhakika wa maisha, yeye na familia yake ya baadaye.
Katika hali nyingi, mwanamke anapoondoka, hachukui uamuzi huo kwa wepesi. Huwa tayari amevumilia kwa muda mrefu, amesamehe mara nyingi, na amejaribu kuamini hata pale dalili zilipoonyesha kutokuwa na mwelekeo. Lakini anapofika umri au hatua ambayo inamtaka awe na uthabiti wa maisha, huanza kutambua kuwa anahitaji mwanaume wa vitendo, si mchumba wa maneno. Ndiyo maana wakati mwingine huonekana kana kwamba amemsaliti mwanaume aliyempenda, ilhali ukweli ni kwamba aliamua kujinusuru dhidi ya maisha ya sintofahamu.
Mwanamke ni kiumbe wa kipekee; anaweza kuendelea kuwepo kimwili katika uhusiano, lakini moyo wake ukaanza kujitenga taratibu. Hucheka, huongea, huendelea na maisha ya kawaida, lakini ndani yake tayari amechoka. Anapofika hatua ya kuondoka kabisa, mara nyingi huwa tayari amefanya maamuzi yote moyoni. Ndiyo maana kuondoka kwake huonekana kwa ghafla, ilhali kiuhalisia ilikuwa safari ndefu ya maumivu na tafakari ya kina.
Ni muhimu kwa mwanaume kuelewa kuwa kumpa mwanamke maneno matamu au ngono hakumaanishi kumpa maisha. Mwanamke anaweza kufurahia mapenzi ya leo, lakini bado akahitaji uhakika wa kesho. Anahitaji kuona juhudi, mipango, na uwajibikaji unaoonyesha kuwa mwanaume anajua anakoelekea. Pale ambapo hayo hayapo, mwanamke hulazimika kuchagua amani ya maisha yake kuliko hisia zinazomuumiza polepole.
Kwa hiyo, ushauri mkubwa kwa mwanaume ni kupunguza ahadi zisizotekelezeka na kuongeza vitendo vinavyoonekana. Mwanamke hahitaji mwanaume mkamilifu, bali anahitaji mwanaume mwenye mwelekeo, msimamo na uhalisia. Umri na muda wake vinahitaji faraja, uthabiti na usalama wa maisha, si kusubiri kesho ambayo haijawahi kufika. Mwisho wa yote, mwanamke anapoondoka, mara nyingi haondoki kwa sababu hakupenda, bali kwa sababu alichagua maisha yenye maana na uhakika.
Mr Elimu Jamii
Mr Elimu Jamii
No comments